“Kuanzia sasa jukumu la kukusanya na kusimamia michango ya aina yoyote ile shuleni lifanywe na wazazi wa wanafunzi hao kupitia bodi za shule badala ya walimu na kuanzia sasa mwalimu haruhusiwi kumrudisha nyumbani mwanafunzi mwenye upungufu wa mahitaji ya shule na badala yake amshirikishe mzazi juu ya umuhimu wa mahitaji hayo ili mzazi kwa hiyari yake aweze kutimiza majukumu yake ya msingi kwa mwanae akiwa shuleni”
Hayo ni maneno yaliyozungumzwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi alipokuwa katika ziara yake Kijiji cha Munguli mapema jana ambapo alifika kwa ajili ya kukagua mradi mkubwa wa Maji na kuzindua darasa la kisasa la shule ya Msingi Munguli na Ofisi ya Walimu miradi yote ikiwa imewezeshwa na Mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka nchini Norway yanayojulikana kama ‘Norwegian Church Aid’ (NCA) na ‘4 corners Cultural Program’ (4CCP).
Mhe. Nchimbi ameyapongeza mashirika hayo kwa kuwezesha ujenzi wa miradi mikubwa katika kijiji cha Munguli ambapo aliongeza kuwa undugu huo kati ya Wilaya ya Mkalama na mashirika hayo unapaswa kuenziwa kwa njia ya utunzaji bora wa miradi hiyo ili kuwapa nguvu wafadhili hao kuendelea kuboresha miundombinu mingine iliyopo Wilayani hapa.
“Ninapenda kutoa shukrani zangu za dhati kwenu na mimi huwa napenda kusema kuwa kushukuru ni kuomba tena hivyo ninawaomba kama ilivyowapendeza kwa upande wa Munguli Magharibi, muiangalie Munguli Mashariki kwa jicho hilo hilo kwani nao wanahitaji sana miradi mliyoiweka hapa kwa wenzao” Aliongeza Mhe. Nchimbi.
Suala la upandaji wa Miti ya Korosho na matumizi mazuri ya Fedha zinazotolewa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (TASAF) ni moja ya mambo yaliyosisitizwa na Mhe. Nchimbi katika hotuba yake kijijini hapo ambapo aliagiza wakuu wa shule zote za Msingi na Sekondari kuhakikisha wanapanda korosho katika mashamba ya shule zao na walengwa wote wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii wanatumia fedha hizo kujikwamua kiuchumi badala ya kuzitumia kwenye ulevi na anasa nyingine.
Awali akimkaribisha Mkuu wa Mkoa, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka aliyashukuru Mashirika ya NCA na 4CCP kwa kuwezesha miradi hiyo mikubwa Wilayani kwake ambapo aliwaagiza wananchi wa Kijiji hicho kuhakikisha hawafanyi shughuli za kiuchumi katika maeneo yaliyo karibu na mradi wa Maji ili kuweza kuulinda mradi huo.
Kwa upande wake Afisa Miradi wa Mashirika ya NCA na 4CCP Nelson Faustineamewashukuru viongozi wote wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa ushirikiano Mkubwa waliouonesha katika kipindi chote cha Ujenzi wa Miradi hiyo jambo ambalo alikiri kutolipata kwa kiwango hicho katika maeneo mengine yote waliyotekeleza miradi yao.
“Mkuu wa Wilaya na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama wametuonesha ushirikiano mkubwa sana na ilifikia hatua tulikuwa tunawapigia simu muda wowote tunaaohitaji msaada wao na wao hawakusita kutusaidia” Alisisitiza Faustine.
Mashirika ya NCA na 4CCP yametekeleza miradi hiyo kwa kushirikiana na Kanisa la Kilutheri la Hydom lililopo Wilayani Mbulu Mkoani Manyara.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.