Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Moses Machali amewapongeza wananchi wa Kijiji cha Tumuli, Kata ya Tumuli kwa uamuzi wao wakuanza ujenzi wa zahanati katika kijiji hicho na kuwataka kuendelea na juhudi hizo hadi kukamilisha ujenzi huo ili kusogeza huduma karibu kuepusha changamoto ya kufuata huduma za afya katika kijiji cha Maluga kilichopo Wilaya ya Iramba na kijiji cha Iguguno .
Ameyasema hayo Disemba 06, 2023 katika muendelezo wa ziara zake za kusikiliza na kutatua kero za wananchi katika kijiji cha Tumuli, Kata ya Tumuli Wilayani Mkalama.
‘’Niwapongeze wananchi wa Tumuli kwa uamuzi wenu wa kuanzisha ujenzi wa zahanati hii mmefanya uamuzi mzuri sana niwapongeze sana , niwaambieni tu maendeleo hayaletwi na serikali pekee’’ Alisisitiza Mhe. Machali.
Amewasisitiza kuharakisha kukamilisha ujenzi huo ili serikali iweze kuwaletea wataalamu pamoja na vifaa tiba katika kusogeza huduma karibu na kuwaondolea adha ya kufuata huduma mbali.
Aidha Mhe. Machali aliwataka kuwashirikisha wataalamu wa majengo kukagua na kuthibiti viwango na ubora wa jengo hilo na kuepuka makosa na hasara iliojitokeza katika jengo la awali ambalo lilikuwa hatua ya ukamilishaji na kuonekana halina ubora .
‘’Nitawaletea msanifu majengo ‘Quantity Surveyor’ kuja kulikagua jengo hili ili kuepusha makossa yaliyojitokeza hapo awali katika jengo la zahanati ambalo lilibainika halina ubora na halifai kwa matumizi’’ aliongeza Mhe. Machali.
Ameendelea kuwasisitiza wananchi kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali kuchangia maendeleo mbalimbali huku akiwataka kuendelea kuwapa ushirikiano watendaji na wataalamu ambao serikali imewaamini kwaajili ya kuwatumikia ambapo amesema mwananchi asiyechangia maendeleo yao hafai kutembea pamoja katika safari ya mafanikio.
Katika hatua nyingine Mhe. Machali ameongeza kuwa serikali inahakikisha inatatua changamoto katika sekta mbalimbali ikiwepo Afya, Kilimo,mifugo na uvuvi, Elimu, Maji , barabara ndio maana amekuwa na utaratibu wa kutembea kila kijiji kwaajili ya kusikiliza na kutatua changamoto zinazowakabili.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.