Naibu Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Dr. Sweetbert Zakaria Mkama ametembelea na kukagua miradi inayotekelezwa kupitia Mradi wa kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa chakula katika maeneo kame Wilayani Mkalama kwa Vijiji vya Munguli, Nyahaa,pamoja na Lugongo ambapo ametaka kuongeza usimamizi katika miradi hiyo ambayo inaonekana kusua sua kukamilika.
Akiongea katika ziara hiyo Mei 17 2023 Dr. Mkama amesema serikali inatoa fedha nyingi kwaajili ya kuharakisha maendeleo kwa wananchi lakini wasimamizi wa Miradi wamekuwa wakikwamisha miradi kukamilika kwa wakati .
‘’Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Mama Yetu Dkt. Samia Suluhu Hassani inatoa fedha hizi kwaajili ya kuleta maendeleo kwa wananchi lakini kwanini mnataka kumkwamisha mama?mbona miradi mingine mnakamilisha kwa wakati? Kwanini hii ya mazingira? Fedha zote anatoa Mama hivyo hakuna miradi ‘Grade A, B wala F’ serikali ikitoa fedha lazima miradi yote ipewe kipaumbele kama ilivyo kwa miradi mingine” Alisisitiza Dr.Mkama.
Dr. Mkama ametaka thamani ya pesa iendane na miradi inayotekelezwa pamoja na michoro yote ‘BOQ’ ambapo amewataka kufuata maelekezo nasio kufanya tofauti na mwongozo unavyosema .
Pamoja na hayo aliwataka wasimamizi wa miradi hiyo kuongeza kasi ya usimamizi ili miradi hiyo ilete tija kwa wananchi ambao wamesubiri kwa shauku kubwa waweze kujiletea maendeleo pamoja na kukuza uchumi na kuwanasua katika hali ngumu ya maisha.
Miradi iliyotembelewa ni pamoja na ujenzi wa Jengo la kuchakata asali katika Kitongiji cha Kipamba Kijiji cha Munguli, Ukarabati wa Josho katika Kijiji cha Nyahaa pamoja na Ujenzi wa Jengo la kuchakata Nafaka katika Kijiji cha Lungongo.
Ziara hii inakuja siku chache baada ya ziara ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Sulemani Jafo kutembelea Wilayani hapa na kukagua miradi ya kurejesha Ardhi iliyoharibika na kuongeza usalama wa Chakula katika maeneo kame.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.