Siku ya jumatatu ya wiki hii (Julai 3,2017) Wilaya ya Mkalama ilikimbiza Mwenge wa Uhuru baada ya kuupokea kutoka Wilaya ya Iramba ambapo ulikimbizwa katika Miradi 7 iliyopo Wilayani hapa huku minne ikiwa ni ya kuwekwa jiwe la msingi, miwili ya kuzinduliwa na mmoja wa kukaguliwa/kuonwa.
Miradi hiyo ni pamoja na wa ujenzi wa bweni kubwa la wanafunzi, bwalo la chakula na vyoo unaoendelea katika shule ya sekondari Iguguno, mradi wa maji safi uliopo katika kijiji cha Mnolo, Mradi wa Kiwanda cha kukamua mafuta ya alizeti na ufugaji wa nyuki uliopo katika kijiji cha Kinyangiri, mradi wa Ujenzi wa Ukumbi mkubwa wa Mikutano na hadhara mbalimbali uliopo katika Ofisi za Halmashauri ya Wilaya katika kijiji cha Nduguti, mradi wa ujenzi wa barabara ya Kijiji cha Mwando mpaka kijiji cha Nkalakala na mradi wa soko la Vitunguu uliopo katika kijiji cha Dominiki.
Jumla ya gharama ya miradi yote hiyo mpaka kukamilika kwake ni shilingi 5,197,865,111 ambapo michango iliyotolewa kupitia nguvu za wananchi ni shilingi 35,770,000 huku fedha iliyotolewa na serikali kuu ikiwa ni shilingi 1,694,878,769 Upande wa Halmashauri ya Wilaya imetoa shilingi 9,580,000 huku wahisani wakitoa shilingi 467,045,111.
Katika miradi yote hiyo Kiongozi wa mbio za Mwenge kitaifa Ndugu Amour H. Amour amesisitiza juu ya matumizi bora ya fedha za serikali ambapo aliagiza miradi yote ilingane na thamani ya pesa iliyotumika kuikamilisha.
“Niwapongeze sana kwa kuwa na jengo zuri na kisasa kuliko yote katika Maeneo ambayo Mwenge umeshapita na naomba nisisitize juu ya utoaji huduma bora zenye kufuata weledi kwa wananchi ili thamani na uzuri wa jengo hili uendane na huduma wanazopata wananchi huku mkizingatia kuwa madaraka mliyonayo yanatokana na uwepo wa wananchi hawa” Aliongeza Amour.
Akiwa katika mradi wa ujenzi wa bweni, bwalo na vyoo ambao umegharimu zaidi ya shilingi milioni 400, katika shule ya Iguguno Amour alisifu jitihada zilizofanywa na uongozi wa Halmashauri ya Wilaya kupitia uongozi wa Shule hiyo kwa kazi nzuri ya kuhakikisha wanafunzi wa shule hiyo pekee yenye wanafunzi wa kidato cha tano na sita katika Wilaya ya Mkalama wanakuwa na mazingira mazuri kuanzia sehemu ya kula mpaka kulala ambapo aliwataka wanafunzi hao kusoma kwa bidii.
Mara baada ya kumaliza mbio zake katika Wilaya ya Mkalama, Mwenge wa Uhuru ulikabidhiwa katika Mkoa wa Simiyu makabidhiano yaliyofanyika katika kijiji cha Bukundi wilayani Meatu siku ya Jumanne Julai 4, 2017.
Mwenge wa Uhuru kwa Mwaka 2017 umebeba ujumbe unaosema “Shiriki Kukuza Uchumi wa Viwanda kwa maendeleo ya nchi yetu”
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.