“Umoja wa Nchi za Afrika umeichagua Tanzania kama kitovu cha Ukombozi wa bara la Afrika na kitajengwa kituo maalum cha kumbukumbu za Ukombozi wa bara la Afrika jijini Dar-es-salaam”
Ni kauli iliyotolewa na Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo Mhe. Harrison Mwakyembe wakati wa ziara yake aliyoifanya muda mfupi uliopita Wilayani hapa ambapo pamoja na mambo mengine alitembelea Uwanja wa kisasa wa Mpira wa Miguu unaojengwa katika kijiji cha Maziliga na kwenda kwenye boma la Wajerumani lililopo katika kijiji cha Ibaga.
“Hivi karibuni tumepeleka wachezaji wetu wa timu ya Ngorongoro kwenda kujipima kwenye michuano ya Uefa kwa wachezaji wanaendana nao umri na wamerudi wakiwa wamejifunza mambo mengi kwa sababu pamoja na kufungwa na baadhi ya nchi pia kuna nchi nyingine zilizopiga hatua upande wa soka walizifunga ikiwemo Senegal na Australia” Alisema Mhe. Mwakyembe.
Akiwa kwenye Uwanja wa Maziliga, Mhe. Mwakyembe alikipongeza Chama cha Mapinduzi na wananchi wote wanaoendelea kuchangia ujenzi wa Uwanja huo ambapo aliahidi kutuma wataalam kutoka baraza la Michezo la taifa (BMT) kwa ajili ya kuja kutoa msaada zaidi wa kitaalam ili kuufanya uwe wa kisasa zaidi baada ya kukamilika kwake.
Baaada ya kufika Ibaga Mhe. Mwakyembe pamoja na kusifu na kupongeza uwepo wa malikale na vivutio vya Utalii Wilayani Mkalama pia alionesha kusikitishwa na uharibifu uliofanywa na wananchi kwenye boma la wajerumani liilopo Ibaga ambao walichimba sehemu kubwa ya eneo la boma hilo kutokana na Imani kuwa Wajerumani walizika tunu mbalimbali chini ya ardhi ya eneo hilo.
“Kwa kweli thamani ya uharibifu mlioufanya hapa ni kubwa kuliko hizo tunu mlizokuwa mnazitafuta kwa sababu mmefuta historia nzuri ambayo hata wajukuu zenu wangekuja kujifunza na kujua asili yao” Alisisitiza Mhe. Mwakyembe.
Mhe. Mwakyembe aliahidi Wizara yake itahakikisha boma hilo linajengwa na kurejeshwa katika asili yake ili kuwawezesha vizazi vilivyopo na vijavyo kujua kwa undani juu ya asili yao.
Awali akimpa taarifa fupi baada ya kumpokea Mhe. Mwakyembe, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Jackson Masaka alisema kuwa Mkalama ni miongoni mwa wilaya zilizojaaliwa kuwa na tunu ya makabila ya asili kabisa barani Afrika yanayoendelea kutunza mla na desturi zake mpaka leo huku akitoa mfano wa kabila la Wahadzabe.
Mara baada ya kutoka katika kijiji cha Ibaga Mhe. Mwakyembe alieleke Wilayani Ikungi kwa ajili ya kuendelea na ziara yake.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.