“Badili fikra kufikia usawa wa kijinsia kwa maendeleo endelevu” Ni kauli mbiu iliyotumika katika maadhimisho ya mwaka huu ya siku ya wanawake duniani ambapo kwa Wilaya ya Mkalama sherehe za maadhimisho hayo zimefanyika katika kata ya Miganga.
Maadhimisho hayo ambayo kwa kiasi kikubwa yalipambwa na burudani mbalimbali zilizobeba ujumbe wa kumsifu mwanamke yalitanguliwa na zoezi la upandaji wa miche ya miti kuzunguka eneo la ujenzi wa kituo cha Afya cha Miganga lililoongozwa na Mgeni rasmi wa sikukuu hiyo Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka.
Akihutubia wananchi waliojitokeza katika maadhimisho hayo, Mhe. Masaka alisema kuwa serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli imewawezesha kwa kiasi kikubwa wanawake kuonesha uwezo wao katika nyanja mbalimbali za uongozi huku akitoa mfano wa viongozi mbalimbali wanawake walioaminiwa na Rais akiwepo Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, Naibu spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Tulia Ackson na wengine wengi.
“Kwa mantiki hii Mhe. Rais ameshatuthibitishia kuwa kumbe wanawake pia wanaweza kufanya kazi vizuri kama walivyo wanaume hivyo naagiza hata kwenye shule zetu kuanzia sasa tuondokane na maagizo yanayolenga kuonesha ubaguzi wa kijinsia kwa sababu anachokiweza mwanaume na mwanamke anaweza kufanya” Aliongeza Mhe. Masaka.
Mhe. Masaka pia alitumia fursa hiyo kuwaonya wale wote wanaojihusisha na kuwapa ujauzito wanafunzi ambapo alisema kuwa mtu yoyote atakayebainika kufanya kitendo hicho atashughulikiwa bila kujali itikadi zake za siasa, dini na kabila.
“Kama wewe ni Mwana-CCM na umebainika kumpa ujauzito mwanafunzi tutakushughulikia bila kujali nafasi yako kwenye chama na hali itakuwa hivyo pia hata katika upande wa dini na makabila hatutamuacha mtu” Alisisitiza Mhe. Masaka.
Mhe. Masaka alihitimisha hotuba yake kwa kuwapongeza wanawake kwa kazi nzuri za maendeleo wanazofanya ambapo aliwahimiza kuendelea kujiamini, kujituma na kuwa na uthubutu wa kutumia fursa zilizopo.
Siku ya Wanawake duniani huadhimishwa kila ifikapo Machi 8 ya kila mwaka ambapo huambatana na kauli mbiu mbalimbali zinazolenga kumuinua mwanamke.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.