Zoezi la kupiga chapa ng’ombe kwa Wilaya ya Mkalama limehitimishwa mapema leo katika kijijicha Gumanga ambapo jumla ya Ng’ombe 192,900 ikiwa ni zaidi ya lengo la awali lililolenga kupiga chapa jumla ya ngombe 127,849.
Akisoma taarifa fupi ya utekelezaji wa zoezi, Afisa Mifugo wa Wilaya ya Mkalama Elias Mbwambo amesema utekelezaji wa zoezi hilo unatokana na sheria namba 12 ya Mwaka 2010 ya usajili, ufuatiliaji na utambuzi wa mifugo ikichagizwa na takwa la soko la kimataifa ambapo ili mifugo iingie katika soko hilo ni lazima ijulikane mahali ilipotoka.
Mbwambo amesema kuwa katika zoezi hili kila mfugaji alitakiwa kulipia shilingi 500 kama gharama ya chapa ambapo fedha hizo zilikuwa zikitumika kwa ajili ya kuratibu zoezi zima mpaka kukamilika kwake.
“Usajili huu umefanyika kwa kutumia code zilizotolewa na Wizara ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi ambazo ni T MKL na code za vijiji zilizotolewa na Wilaya ambapo vijiji vilipangwa kwa mpangilio wa herufi kuanzia kijiji namba moja hadi 70 na chapa hiyo iliwekwa mguu wa nyuma kulia katikati ya goti na paja” Alisema Mbwambo.
Aidha Mbwambo ameongeza kuwa wafugaji wanaruhusiwa kuwa na alama zao za utambuzi ambapo zitatakiwa kusajiliwa kwanza ndipo wazitumie bila kuathiri zile za serikali na alama hizo zitawekwa mkono wa mbele upande wa Kulia.
Akizungumza muda mfupi kabla ya kufunga rasmi zoezi hilo kwa awamu hii, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka amemuagiza Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kuhakikisha anatenga maeneo ya kulisha mifugo hiyo ili kuondokana na migogoro baina ya wafugaji na wakulima.
“Kumekuwa na mazoea ukifika msimu wa masika maeneo yote huwa yanalimwa na kusababisha mifugo kukosa maeneo ya chakula jambo ambalo huweza kusababisha mgogoro baina ya mkulima na mfugaji” Alisema Masaka.
Mhe. Masaka ametoa agizo kwa serikali za vijiji kuwa endapo ng’ombe asiye na chapa atachinjwa, kuuzwa au kusafirishwa nje ya Wilaya hatua za kisheria zichukuliwe dhidi ya mwenye ng’ombe, mchinjaji na mnunuzi wa ng’ombe huyo.
“Wananchi watumie mifugo yao kwa kujiendeleza na kuboresha hali za maisha kwa kufanya shughuli za maendeleo” Alimalizia Mhe. Masaka.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.