Wilaya ya Mkalama leo imeungana na maeneo mengine yote kusherehekea siku ya kimataifa ya wanawake iliyofanyika katika kijiji cha Mwando yakiwa ni maadhimisho ya tano ya sikukuu hiyo tangu kuanzishwa kwa Wilaya hii.
Katika maadhimisho hayo ambayo mwaka huu yamebebwa na kauli mbiu ya kitaifa isemayo “Kuelekea Uchumi wa Viwanda tuimarishe usawa wa kijinsia na uwezeshaji wa Wanawake” viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Mkalama na Mkoa wa Singida kwa ujumla walitumia fursa hiyo kuhamasisha wanawake kujitokeza katika fursa mbalimbali na kupiga vita hali ya utegemezi dhidi ya wanaume.
Mbunge wa Viti maalum Mkoa wa Singida Mhe. Asha-Rose Matembe aliwaasa wanawake wote Wilayani Mkalama kujunga kwenye Vikundi ili waweze kukidhi vigezo vya kupatiwa mikopo ya Serikali na taasisi mbalimbali za fedha.
“Niwaombe Sido na taasisi mbalimbali za fedha watembelee vikundi vya wanawake na kutoa elimu ya Ujasiriamali ili fedha wanazokopeshwa ziweze kuwa na tija” Alisisitiza Mhe. Matembe.
Mhe. Matembe pia amepongeza jitihada za wazi zilizooneshwa na wananchi wa Kijiji cha Mwando kwa Kujenga Zahanati ambapo aliunga mkono jitihada hizo kwa kuwaahidi kuchangia mifuko 50 ya Saruji huku 30 akiikabidhi hapo hapo na mingine 20 kuahidi kuitoa ndani ya siku chache zijazo.
Awali kabla ya Kumkaribisha Mgeni Rasmi wa maadhimisho hayo, Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhandisi Godfrey Sanga aliainisha jitihada mbalimbali ambazo serikali imezifanya ndani ya Wilaya ya Mkalama katika kuinua Ustawi wa wanawake ambapo mbali na Asilimia 5 inayokwenda kwenye vikundi vya wanawake vilivyosajiliwa kila Mwezi, Serikali pia inatarajia kukamilisha wodi ya wanawake iliyopo katika Zahanati ya Nduguti ndani ya Siku 60 kuanzia sasa.
“Pia ndani ya Miezi miwili ijayo tunatarajia kukamilisha Ujenzi wa Kituo cha Afya cha Kinyambuli ambacho ndani yake kuna Chumba kikubwa cha Upasuaji kwa wanawake wajawazito jambo ambalo litazidi kuhakikisha usalama wa afya za wanawake waliopo Wilayani Mkalama” Alisisitiza Sanga.
Sanga aliongeza kuwa Bweni la Wanafunzi wa kike katika Shule ya Sekondari Nduguti linatarajiwa kukamilika muda wowote kuanzia hivi sasa hivyo kuanzia Muhula ujao wanafunzi wa Kike wote waliopo shuleni hapo watakuwa wakiishi bwenini jambo litakaloongeza usalama wa watoto wa kike pindi wakiwa shule.
Katika hotuba yake, Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka ameainisha aina mbalimbali za Unyanyasaji wa wanawake unaoendelea katika jamii likiwemo suala la ndugu wa Marehemu kuchukua Mali pindi mwanamke anapofiwa na mumewe.
“Jambo hili katika Wilaya ya Mkalama sitaki kulisikia na naagiza hatua kali za kisheria zichukuliwe dhidi ya watakaobainika kufanya hivyo” Aliongeza Mhe.Masaka.
Mhe. Masaka aliongeza kuwa kumekuwa na tabia isiyopendeza kwa baadhi ya wanaume ambapo wamekuwa wakiwalaumu wake zao pindi watoto wanapoharibikiwa kimaadili huku wakisahau kuwa jukumu la malezi ya watoto ni la baba na mama kwa pamoja na si mama peke yake.
“Lakini bado kuna baadhi ya kaya ambazo mpaka leo hazimpi mwanamke haki ya kupanga uzazi na bado jamii imekuwa ikifumbia macho badala ya kutoa ushauri unaofaa jambo ambalo linasababisha wanawake kuchoka sana kwa kuzaa mfululizo bila kufuata uzazi wa mpango” Alisema Mhe. Masaka.
Mhe. Masaka alihitimisha hotuba yake kwa kuwataka wanawake wote Wilayani Mkalama kutoona ni jambo la kawaida kwa watoto wao wa kike kupata ujauzito wakiwa shuleni kwa sababu takwimu zinaonesha kiwango cha watoto wa kike wanaopata ujauzito wakiwa Shuleni ni asilimia moja tu hivyo ni lazima wazazi wa watoto hao waungane na hiyo asilimia 99 ili kutokomeza kabisa hali hiyo.
“Mpaka sasa Jumla ya Kesi tatu za ubakaji zimeshafikishwa Mahakamani Wilayani hapa na wahusika wote waliokutwa na hatia wamehukumiwa vifungo” Alimalizia Mhe. Masaka.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.