“Elimu ni moyo wa uhakika na hakikisho la uhai wa maendeleo endelevu ya familia, jamii na Taifa kwa ujumla”
Hayo ni maneno yaliyotamkwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Juma la Elimu tukio lililofanyika katika viwanja vya Ofisi ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.
Mhe. Nchimbi ambaye alimwakilisha Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI) Mhe. Selemani Jafo, alitumia fursa hiyo kuwashukuru wadau wote wa elimu chini ya mwamvuli wa Mtandao wa Elimu Tanzania (TenMet) ambapo aliwataka watumie maadhimisho ya mwaka ujao kutoa majibu ya tathmini ya utekelezaji wa changamoto zote walizoziona katika Wilaya za Nanyumbu na Mkalama.
“Haiwezekani kila mwaka muwe mnazungumzia changamoto za aina moja hivyo ni lazima muweke mpango mzuri wa kufanya ufuatiliaji wa karibu wa utekelezaji wa changamoto zote mlizoziainisha” Alisisitiza Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi aliushukuru uongozi na wananchi wa Mkalama kwa ujumla kwa kuahidi kubadilisha matokeo waliyoyapata mwaka jana ambapo aliwasisitiza wajikite zaidi kwenye mabadiliko ya vitendo badala ya maneno.
Kabla ya kutangaza kufunga maadhimisho ya juma la Elimu kwa mwaka huu, Mhe. Nchimbi aliendesha harambee ya kuchangia elimu Wilayani hapa ambapo jumla ya shilling 600,000 zilipatikana.
Awali akizungumza maneno machache kabla ya kumkaribisha mgeni rasmi, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka alisema kuwa TenMet waliamini Mkalama bado ipo hai ndio maana walifika kuisaidia kuainisha sababu mbalimbali zilizosababisha kutokuwa na matokeo mazuri ambapo aliwaahidi kuwa Wilaya yake haitofanya vibaya tena.
Wakati huo huo Mhe. Masaka alitumia fursa hiyo kuwatakia kila la kheri waislam wote wa Wilaya ya Mkalama katika Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani ambapo aliwataka wafanyabiashara wote Wilayani hapa kutopandisha bei za vyakula ambavyo hutumiwa kama futari na daku katika kipindi hiki.
“Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya itafuatilia kwa karibu sana utekelezaji wa agizo hili na atakayekiuka hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi yake” Aliongeza Mhe. Masaka.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.