MIRADI YA BOOST MINGI IMEKAMILIA KWA 100% MICHACHE IPO KWENYE 90% HADI 95%" RC SERUKAMBA '
MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amefanya ziara ya kukagua miradi ya ujenzi shule mpya za msingi zinazojengwa kwa fedha za BOOST na kuagiza viongozi wa Halmashauri zote za Wilaya Mkoani hapa kuhakikisha ujenzi huo unakamilika haraka ili shule hizo zianze kutoa huduma.
Serukamba ameyasema hayo hivi karibuni baada ya kutembelea miradi ya Boost katika Halmashauri za Wilaya za Mkalama, Iramba , Singida Vijijini na Halmashauri ya Manispaa ya Singida.
Katika Halmashauri ya Wilaya Mkalama alitembelea na kukagua ujenzi wa shule mpya ya Ishenga na kuongea na Wananchi ambapo aliwapongeza viongozi wa Wilaya kwa kusimamia vizuri miradi hiyo ambayo mingi imekamilika kwa asilimia 100 na michache ipo kati ya asilimia 90 na 95.
"Nichukue nafasi hii kuwapongeza watendaji wenzangu kwa kweli miradi hii imekwenda vizuri, majukumu yetu tuendelee kuyafanya na niwaombe Madiwani na Wenyeviti wa vijiji wahamisishe wananchi kwa ajili ya kufanya usafi katika shule zilizojengwa ikiwa ni pamoja na kupanda miti kuzunguka shule," alisema Serukamba.
Ameongeza kuwa katika kuhakikisha zoezi la upandaji miti linafanikiwa, wanafunzi wapewe miti ya kupanda na kuisimamia jambo ambalo litazifanya shule hizo kupendeza na kuwa na mazingira mazuri.
Serukamba alisema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan amejipambanua kwa kufanya kazi kubwa sana ya kuendeleza maisha ya watu kuwekeza kwenye maisha ya watu na vitu vinavyohusu watu.
"Kuwekeza kwenye elimu ni kuwekeza kwenye mtu mmoja mmoja, ukiwekeza kwenye afya umewekeza kwenye afya ya mtu mmoja kimsingi Mhe. Rais amefanya kazi kubwa sana sana, pia hajaacha sekta za uchumi kama umeme, barabara kuna kazi kubwa sana imefanyika," alisema Serukamba.
Ameongeza kuwa katika sekta ya umeme Mkoa wa Singida una vijiji 441 itakapofika Juni 2024 kila Kijiji kitakuwa kimepata huduma ya umeme na kumpongeza Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kazi nzuri alizofanya kwa Mkoa wa Singida.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.