Waziri wa Mifugo na Uvuvi Mhe. Abdallah Ulega amesema kuwa uwepo wa madume bora ya kisasa ya Ng’ombe aina ya BORAN yatafungua fursa za kiuchumi kwa wafugaji Wilayani Mkalama kwani itaongeza uzalishaji wa nyama utakaopelekea wafugaji kupata soko ndani na nje ya Nchi .
Ameyasema hayo mapema leo April 6, 2023 katika hafla fupi ya kukabidhi mbegu bora ya madume Arobaini (40) ya Ng’ombe iliyofanyika katika kijiji cha Iguguno Kata ya Iguguno Wilayani Mkalama.
Aidha Mhe . Ulega ameongeza kuwa Serikali imedhamiria kuboresha Sekta ya Mifugo na kuwainua wafugaji ili kuhakikisha wanaongeza kipato chao kupitia mifugo itakayoleta mageuzi kiuchumi kwa mtu mmoja mmoja , Wilaya , Mkoa pamoja na Taifa.
‘’Serikali ya awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kipindi cha miaka miwili imedhamiria kuinua Sekta ya Mifugo Nchini na kutoa zaidi ya Shillingi Million 800 kununua madume bora ya mbegu ya Ng’ombe 366 ambayo leo hii inamgusa hadi mwananchi wa Mkalama lengo likiwa ni kuinua kipato cha mtu mmoja mmoja na kuleta mageuzi ya kiuchumi Wilayani hapa’’ Aliongeza Mhe. Ulega
Aidha alitumia hafla hiyo kuwataka wafugaji kutumia madume hayo vizuri kutokana na malengo yaliyokusudiwa na serikali ili kuunga mkono juhudi hizo zinazokusudia Ng’ombe hao kupandisha Ng’ombe jike ili kuweza kupata mbegu bora itakayoleta faida kwa wafugaji huku akiwaonya kutofanya Ng’ombe hao kuwa kitoeo.
Awali akimkaribisha Waziri, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Mosses Machali ameishukuru serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kutoa madume ya Mbegu 40 katika Wilaya ya Mkalama ambayo yatagaiwa kwa Vikundi Arobaini vya Wafugaji ambapo ameahidi kuwa watahakikisha wanasimamia vizuri Madume hayo ili kufikia malengo tarajiwa ya kuwa na mifugo bora yenye mazao mengi yatakayochangia kuongeza na kukuza Uchumi kwa kaya za wafugaji na uchumi wa taifa na kuongeza uzalishaji wa mazo ya mifugo.
Naye Mbunge wa jimbo la Iramba Mashariki Mhe. Francis Isack Mtinga aliongeza kuwa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ni miongoni mwa Halmashauri 8 kati ya Halmashauri 186 Nchini zilizopokea Madume hayo na kusema ni bahati ya pekee , huku akiomba Serikali kuongeza majosho kwaajili ya kuogesha mifugo ili Wilaya ya Mkalama isiwe na magonjwa yanayoshambulia mifugo sambamba na kuomba ujenzi wa soko kubwa la Mifugo likalopelekea wafugaji kuuza mifugo yao hapa Wilayani na kuongeza vipato vyao pamoja na kuongeza pato la Halmashauri kutokana na kupata ushuru kupitia soko hilo.
Akitoa neno la shukrani kwa niaba ya wananchi Wilayani hapa Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Mhe. James Mkwega ameishukuru serkali kuwajali wananchi wa Wilaya ya Mkalama kupata Mbegu bora za Madume ilikuongeza uzalishaji na upatikanaji wa nyama wilayani hapo ambapo ameomba kujengwa kwa machinjio Wilayani ili Nyama hizo ziweze kuchinjwa mahali pazuri na kwa usalama ili kulinda afya za walaji.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.