Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Twala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhe: George Simbachawene amewaagiza Wakuu wa Mikoa na Wakurugenzi wa Halmashauri wa Wilaya wote kuhakikisha wamewanunulia maafisa habari waliopo katika ofisi zao zana zote zitakazowawezesha kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi na kitaalamu zaidi ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia jana.
Mhe: Simbachawene ameyasema hayo jana wakati wa Hafla ya Uzinduzi wa Tovuti za Mikoa yote na Halmashauri 185 za Tanzania bara ambazo zimetengenezwa kwa ufadhili wa Shirika la Misaada la Marekani (USAID) chini ya usimamizi wa TAMISEMI na Wizara ya Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo.
“Bila kuwapa vitendea kazi maafisa hawa, juhudi zote za serikali katika kukamilisha zoezi hili zitakuwa hazina tija yoyote kwa sababu mtu anayetakiwa kuhakikisha anatimiza lengo tunalolitaka atakuwa hajawezeshwa kikamilifu na ikumbukwe hivi sasa mitandao ya kijamii imemfanya kila mtu kuwa ni mtoa habari hivyo ni lazima tumtofautishe mtaalamu wa serikali na mwandishi wa kwenye mitandao ya jamii” Amesema Simbachawene.
Mhe: Simbachawene Ametoa rai kwa maafisa habari na maafisa Tehama kote nchini kuhakikisha tovuti hizo zinakuwa na taarifa zinazoenda na wakati muda wote na zitoe majibu kwa wananchi walio mbali na ofisi za Serikali katika halmashauri zao.
Naye Waziri wa Habari, Sanaa,Utamaduni na Michezo Mhe: Harrison Mwakyembe amesema kuwa Nchi ya Tanzania jana imeweka historia kubwa sana tangu ilipopata Uhuru kwa sababu haijawahi kupiga hatua hiyo kubwa kabisa.
“Hata Wizara yangu ambayo ipo kwa muda mrefu sana, haikuwa na tovuti yake lakini sasa hivi kupitia zoezi hili imefanikiwa kupata tovuti yake, hongereni sana wote mliofanikisha hili” Amesema Mwakyembe.
Mhe: Mwakyembe aliwataka maafisa habari wote Nchini kuhakikisha tovuti hizo zinakuwa na taarifa sahihi na zinazoenda na wakati ili kukidhi haja ya mwananchi ambaye ndio mlengwa mkuu wa taarifa zinazowekwa humo.
“Tovuti hizi hazitakiwi kugeuka magofu ya kuhifadhia taarifa zilizopitwa na wakati bali zinatakiwa kuwa jokofu la kuhakikisha habari zinakuwa mpya wakati wote na hapa ndio tutatumia kama kipimo kikubwa kwa maafisa habari wote Nchini” Alimalizia Mwakyembe.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.