“Kuanzia sasa Ofisi za upelelezi za Iramba na Mkalama tumekubaliana mashauri ya ubakaji, utiaji mimba wanafunzi na uharibifu wa mali za umma yapelekwe mahakamani moja kwa moja bila kusubiri kukamilika kwa uchunguzi wa polisi ili wahanga wa matukio hayo wakatoe ushahidi mahakamani moja kwa moja na haki iweze kutendeka mapema.”
Kauli hiyo imetolewa na Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya Iramba na Mkalama Mhe. Christopher Charles alipokuwa akizungumza wakati wa maadhimisho ya kilele cha Wiki ya Sheria nchini kwa Wilaya za Mkalama na Iramba yaliyofanyika leo kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.
Mhe. Charles alibainisha kuwa moja ya changamoto kubwa zinazoukabili mhimili wa mahakama kwa mkoa wa Singida ni kukosekana kwa Ofisi ya Mkemia Mkuu ndani ya Mkoa huo jambo linalosababisha kuchelewa kukamilika kwa kesi zinazohitaji uthibitisho kutoka kwenye ofisi yake.
“Mtu anaweza kukamatwa na bangi au unga aina ya “cocaine”, Mahakama haiwezi kutoa hukumu ya kesi hiyo bila kuwa na uthiibitisho kutoka kwa mkemia Mkuu kuwa vithibiti alivyokamatwa navyo ni vya dawa za kulevya au la kwa hiyo mpaka visafirishwe na majibu kurejea inachukua muda mrefu sana” Aliongeza Mhe. Charles.
Mhe. Charles alisema kuwa ili kauli mbiu ya Wiki ya sheria kwa mwaka huu iweze kutimia kwa vitendo ni lazima Mkalama iwe na jengo lake la Mahakama ya Wilaya hivyo aliuomba uongozi wa Wilaya hiyo kuharakisha taratibu za utekelezaji wa azma hiyo inayolenga kuwarahisishia wananchi kupata huduma kwa wakati.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Iramba ambaye pia ni Mwenyekiti wa wakuu wa wilaya zote za Mkoa wa Singida Mhe. Emanuel Luhahula alivipongeza vyombo vya Ulinzi na Usalama Wilayani Iramba kwa kutimiza wajibu wao ipasavyo ambapo aliwataka kuendelea na kasi hiyo ili wananchi wake wapate haki zao kwa wakati.
“Kuna kipindi vitendo vya Rushwa vilikithiri sana Iramba lakini nilipotangaza Vita dhidi ya wanaopokea au kutoa rushwa, vitendo hivyo vimepungua kwa kiasi kikubwa sana” Alisisitiza Mhe. Luhahula.
Naye mgeni rasmi katika Maadhimisho hayo ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Mhandisi Jackson Masaka aliitaka mahakama kuendelea kuhakikisha haki inatendeka katika mashauri mbalimbali yanayosikilizwa ili kuzidi kuongeza Imani ya wananchi dhidi ya mhimili huo muhimu.
Madhimisho ya Wiki ya sheria mwaka 2019 yalibebwa na kauli isemayo “Utoaji haki kwa wakati: Wajibu wa mahakama na wadau”.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.