Katika kuhakikisha wanafunzi wa Wilaya za Mbulu na Mkalama wanaondokana na maradhi yatokanayo na uchafu wa mazingira na ukosefu wa vyoo bora, Shirika lisilokuwa la serikali linalojulikana kama ‘‘Norwegian Church Aid’’ kupitia mradi wake wa 4CCP leo liliratibu kongamano la Usafi lililoshirikisha watendaji mbalimbali wa Halmashauri za Wilaya hizo wakiongozwa na Wakurugenzi watendaji, maafisa elimu msingi na sekondari, maafisa elimu kata, maafisa afya, wakuu wa shule na walimu.
Shirika hilo ambalo tangu mwaka 2016 limekuwa likiendesha kampeni ya kuhakikisha kwenye shule za Wilaya ya Mbulu na Mkalama kunakuwa na matumizi ya maji safi na salama, Usafi wa vyoo, na unawaji mikono kwa usahihi baada ya kutoka chooni inayojulikana kifupi kama “SWASH” liliandaa kongamano hilo kwa lengo la kuwakutanisha wadau wote wanaowajibika na afya za wanafunzi wakiwa shuleni ili kuweza kuwafikishia moja kwa moja changamoto wanazopata katika kuendesha kampeni hiyo.
Akizungumza na viongozi hao mratibu wa kampeni ya “SWASH” kutoka shirika la NCA Bw. Zakayo Makobelo alisema kuwa shirika hilo kwa mwaka huu litajikita kwenye mafunzo ya mtumizi mengine ya maji (Multiple Use of Water), kampeni ya usafi wa mazingira na kuimarisha klabu za Usafi wa Afya pale ambapo zipo na kwenye maeneo ambayo hazipo shirika litahakikisha klabu hizo zinaanzishwa.
Kwa upande wake Mgeni rasmi wa kongamano hilo kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bw. Omary Mtamike aliushukuru uongozi wa shirika hilo kwa kampeni yao ya kuhakikisha afya za wanafunzi wakiwa shuleni zinalindwa ipasavyo ambapo aliwaomba kuongeza klabu nyingi zaidi ili kuondokana kabisa na maradhi yatokanayo na uchafu kwenye shule za Wilaya za Mkalama na Mbulu.
“Wakati mnaanza kampeni hii mwaka 2016, Wilaya ya Mkalama ilikuwa na klabu moja tu ya Swash ambayo ni shule ya Msingi Nkinto lakini mpaka kufikia mwisho wa mwaka jana mlikuwa mmefanikiwa kuongeza klabu nyingine 13 na kuifanya Wilaya ya Mkalama kuwa na klabu 14, Hongereni sana kwa hilo” Aliongeza Bw. Mtamike.
Shirika la NCA limekuwa limekuwa likitekeleza miradi mbalimbali ya kuboresha huduma za jamii katika Wilaya za Mbulu na Mkalama ikiwemo uboreshaji wa miundombinu ya maji, elimu na mazingira.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.