Mapema leo jioni Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe. Daktari Rehema Nchimbi ametembelea banda la halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ambapo ametoa maagizo mbalimbali kwa Mkurugenzi, Mwenyekiti wa Halmashauri na Afisa Kilimo wa Wilaya kuhakikisha maonesho yanayokuja ya Nanenane yanakuwa na tija kubwa hata kwa mwananchi wa Mkalama ambaye hajabahatika kufika katika Maonesho ya kikanda.
Mhe. Nchimbi amesema kuwa Kuanzia sasa Wilaya ya Mkalama itenge eneo kubwa ambalo litawekwa vipando ambavyo vitakuwa hapo kwa kipindi cha Mwaka mzima ili wananchi ambao hawatopata fursa ya kushiriki katika maonesho ya kikanda na kitaifa watumie nafasi hiyo kwenda kujifunza kilimo bora na cha kisasa.
“Ninaposema mwaka mzima namaanisha katika maeneo hayo mfanye utaratibu wa kuchimba visima kwa sababu mvua haipatikani mwaka mzima na hapo wananchi kutoka sehemu mbalimbali watafika na kupata elimu tena vipando hivyo mnaweza kuviita ‘NaneNane Mkalama Mubashara’ mkimaanisha wananchi watakuja kujifunza moja kwa moja kutoka shambani” Amesisitiza Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi amesema kuwa kitendo hicho kitawafanya wananchi wote wa Mkalama waone umuhimu wa sikukuu ya NaneNane kwa sababu pamoja na kutofika katika maonesho ya kikanda na kitaifa bado watakuwa wamepata elimu inayofanana na wale waliohudhuria maonesho hayo kikanda na kitaifa.
“Ikifika Mwezi Septemba nitafuatilia hili ili nijue kama utekelezaji wake umeanza” Ameongeza Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi pia ameagiza halmashauri ya Wilaya ya Mkalama ihakikishe imetangaza bidhaa zake kila inapotimia robo mwaka na bidhaa hizo zisiishie kutangazwa katika redio za mikoani tu bali ununuliwe muda katika vituo vya Televisheni pia.
“Kupitia vipindi hivyo tangazeni kila kinachozalishwa Mkalama vikiwemo vitunguu, asali, nyanya na kwa kufanya hivyo mtakuwa mmetangaza soko la Mkalama sio tu kitaifa bali kimataifa” Amesisitiza Mhe. Nchimbi.
Mhe. Nchimbi amesifia Vitunguu vinavyozalishwa katika Wilaya ya Mkalama ambapo amesema vina ubora wa kimataifa na hata sokoni ndio vitunguu vinavyopewa kipaumbele kuliko vitunguu vinavyozalishwa katika maeneo mengine.
“Kuna baba mmoja ni mstaafu wa jeshi alilima vitunguu katika Mkoa wa Morogoro tena vitunguu vizuri tu lakini alipovipeleka sokoni alikataliwa na kuambiwa vitunguu pekee vinavyonunuliwa hapo ni vile vinavyotoka Mkoani Singida kwa hiyo tangazeni sana bidhaa zenu kwa sababu zina thamani kubwa sana sokoni” Alimalizia Mhe. Nchimbi.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.