Maafisa elimu, Waratibu elimu Kata pamoja na walimu wote wametakiwa kutathimini utendaji kazi wao na kuekeleza nguvu zao katika majukumu yao ili kuhakikisha wanainua kiwango cha taaluma wilayani Mkalama na kuongeza ufaulu.
Kauli hiyo imetolewa mapema leo Disemba 21, 2023 na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Moses Machali katika kikao cha tathimini ya ufaulu wa wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi iliyofanyika katika ukumbi wa Sheketela uliopo Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.
Mhe. Machali amesema kuwa endapo kila mmoja kwa nafasi yake atasimamia majukumu kikamilifu watachoche ongezeko la ufaulu kwa wanafunzi pamoja na kujiweka kwenye nafasi nzuri Kimkoa.
‘Nendeni mkasimamie majukumu yenu kikamilifu Afisa elimu ukitimiza majukumu, Mratibu elimu kata na walimu kwa pamoja mkiwajibika kwa nafasi zenu mtachochea ufaulu Wilayani hapa’’ Mhe. Moses Machali
Pamoja na hayo Mhe. Machali amewataka waratibu elimu na walimu wa shule zote kutumia Ardhi ya shule katika kipindi hiki cha Masika kulima mazao kwaajili ya chakula cha wanafunzi yatakayopelekea kupata chakula shuleni kwa wanafunzi wote ili kupata utulivu wa akili wanapokuwa masomoni.
Aidha, Mhe. Machali amewapa mwezi mmoja waratibu elimu wote wanaoishi Nje ya maeneo yao ya kazi kuishi mahala wanakufanyia kazi ili kuongeza ufanisi wa usimamizi wa majukumu yao.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Asia Messos amesema kama Wilaya imejiwekea mikakati ya kuimarisha na kuboresha usimamizi wa mifumo ya ufuatiliaji ikiwa ni pamoja na kutoa motisha kwa wanafunzi na walimu wanaofanya vizuri katika taaluma, pamoja na kuwatambua wanaofanya vibaya kwa kuwapa zawadi hasi itakayowafanya wajitathimini na kuongeza juhudi.
Bi. Messos amewaagiza watendaji wa kata kushirikiana na waratibu elimu pamoja na kamati za shule kuwachukulia hatua za kisheria wazazi wanaoshindwa kusimamia mahudhurio ya watoto wao ili kuondoa tatizo la utoro kwa wanafunzi ambapo imeonekana ndio tatizo kubwa linalochangia kushuka kwa kiwango cha ufaulu Wilayani hapa.
Awali akisoma taarifa Kaimu Afisa Elimu Shule ya Msingi Mwl. Amina Irumba, amesema kuwa Halmashauri imeongeza ufaulu kwa asilimia 2.7 kwa kupata 68.30% mwaka 2023 ukilinganisha na mwaka 2022 ambapo ufaulu ulikuwa 65.52% ambapo ameongeza kuwa ufaulu kimasomo unaonyesha watahiniwa wamefaulu kwa kiwango cha juu kwa somo la Kiswahili 77% huku somo la Kiingereza na Hisabati ikiwa chini ya 50%.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.