Mkuu wa wilaya ya Mkalama Mhe. Sophia Kizigo amewataka wazazi kuwekeza kwenye elimu ili kuwa na Taifa la wasomi watakaoshika nyadhifa mbalimbali Nchini.
Mhe. Kizigo ameyasema hayo mapema leo Disemba 22 2022 katika hafla ya kupokea madarasa 18 wilayani hapo katika Shule ya Sekondari Iguguno iliyopo Kata ya Iguguno.
Aidha Mhe. Kizigo amewataka wazazi wote Wilayani kwake kuunga juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita ambayo imekuwa ikitoa fedha nyingi katika Miradi ya Elimu kwa kuhakikisha ifikapo mwezi Januari mwakani kila mtoto aliyechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza anaripoti shuleni mapema.
‘’Serikali ya awamu ya sita inatujali sana Wananchi wa Wilaya ya Mkalama leo nimepokea madarasa 18 na Ofisi moja ya walimu hakika Mama ameupiga mwingi ninaomba tuhakikishe tunawekeza kwenye elimu, unajisikiaje Mkuu wa wilaya akatoka mkalama? Mtajisikiaje Watoto wenu wa Mkalama wakawa Mahakimu na wataalamu wa kilimo watakaolima kwa tija kwa masilahi ya Wilaya?..Amesema Mhe. Kizigo
Mhe. Kizigo amewataka wazazi wilayani kwake kutowatumikisha watoto kwenye shughuli mbalimbali za kiuchumi ambapo amebainisha kuwa kufanya hivyo ni kurudisha nyuma juhudi za Serikali ambazo zinalenga kutoa elimu bora kwa watoto.
‘’Ninaomba mtafute watu wengine wa kuchunga sio Watoto wenu waacheni waende shule la sivyo madarasa haya mengi niliyopokea leo yatakosa maana kama Watoto wenu hawataenda Shule’’ Aliongeza Mhe. Kizigo.
Awali akitoa taarifa ya utekelezaji wa ujenzi wa madarasa hayo Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama Bi. Asia Messos amesema Halmasahauri yake ilipokea fedha kiasi cha Shilingi Milioni 340 kwa ajili ya ujenzi wa vyumba 17 vya madarasa ya wanafunzi wa kidato cha kwanza waliochaguliwa kujiunga na Shule kwa mwaka 2023 na tayari madarasa hayo yamekamilika na yapo tayari kutumika.
Aidha Bi Mesos ameongeza kuwa kutokana na ushiriki wa Wananchi kujitoa nguvu kazi fedha zilizotolewa zimechonga viti na meza seti 375, kuongeza chumba kimoja cha darasa katika Shule ya Sekondari Iguguno pamoja na ofisi moja ya walimu hivyo kufanya jumla ya madarasa 18 na Ofisi ya walimu.
Nao baadhi ya wananchi walioshiriki tukio hilo wameishukuru serikali ya awamu ya Sita kwa kujenga madarasa hayo ambayo wamedai yatainua kiwango cha taaluma Wilayani Mkalama huku wakiiomba serikali kuongeza walimu ili kuweka uwiano sawa kati ya wanafunzi na walimu.
Shule zilizopata Mradi huo ni Shule ya Sekondari Chemchem iliyopo kata ya Mpambala, Malaja iliyopo kata ya Nkalakala, Shule ya Sekondari Seth Benjamini iliyopo kata ya Nkalakala, Selenge Kata ya Mwanga, Gracemesaki kata ya Kinampundu, Kikhonda Kata ya Kikhonda, Kinto Kata ya Nkinto, Iguguno kata ya Iguguno, Kinyangiri Kata ya Kinyangiri pamoja na Shule ya Sekondari ya Ibaga Kata ya Ibaga.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.