KAMPENI YA MSAADA WA KISHERIA IMEKUJA KWA MUDA MUAFAKA' WANANCHI MPAMBALA WANENA'
Wananchi wa Kata ya Mpambala katika Vijiji vya Mpambala, Mkiko na Lugongo wamemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia Kampeni yake ya msaada wa kisheria (Mama Samia Legal Aid Compaign) kwani imelenga kutatua matatizo yao mbalimbali ambayo walikuwa hawajui pakuyapeleka.
Wamesema hayo mapema leo Januari 12, 2024 kwa majira tofauti tofauti baada ya timu ya wataalamu kufika katika maeneo hayo na kueleza namna Kampeni hiyo itakavyoenda kufanya kazi hususani kutatua migogoro kwenye ngazi ya jamii ikiwepo inayohusu masuala ya Ardhi, Ndoa , Mirathi pamoja na matunzo kwa watoto.
Pamoja na hayo wamesema kuwa kampeni hiyo imefika kwao kwa muda muafaka kwani walikuwa wanashindwa ni wapi wapeleke matatizo yao na kuongeza kuwa watatumia vyombo vya utatuzi vilivyopo kwenye vijiji pamoja na kata zao ikiwa ni pamoja na kutumia vizuri mabaraza ya kata katika kutatua migogoro ya Ardhi ambayo imeonekana kwa asilimia kubwa imekithiri katika maeneo yao pamoja na kujua namna ya kuripoti vitendo vya ukatili ambao waathirika wakuu wametajwa kuwa ni watoto na wanawake.
Awali akitambulisha Kampeni hiyo Bw.Antony Elias kutoka Wizara ya katiba na sheria amesema kuwa serikali ya awamu ya sita imefanya mambo mengi katika nyaja mbalimbali lakini ikaona ni vyema ije na kampeni ya msaada wa kisheria kwa wananchi ambayo itatolewa bure kabisa.
‘’Serikali ya awamu ya sita imefanya mambo mengi lakini ikaona bado kuna changamoto kwenye masuala ya sheria ndio maana ikaamua kuja na kampeni hii maalumu inayohusu masuala ya kisheria’’ alisisitiza Bw Elias.
Aidha Bw . Elias amesema kampeni ya huduma ya msaada wa kisheria ya Mama Samia kwa Wilaya ya Mkalama imelenga kufika katika Kata 10 na vijiji 30 ambapo amewaomba wananchi wa maeneo husika kujitokeza kwa wingi kupata elimu ya masuala ya kisheria,
Kampeni hii ya huduma ya msaada wa kisheria Kitaifa ilizinduliwa April 27, 2023 ambapo mgeni Rasmi alikuwa Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe, Kassim Majaliwa na kwa Mkoa wa Singida imezinduliwa Januari 10 , 2024 na Waziri wa Katiba na Sheria Dkt. Pindi Chana na tayari ishafika katika Mikoa sita ikiwepo Dodoma, Manyara, Shinyanga, Ruvuma, Simiyu pamoja na Singida.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.