JUNI 20, 2023 MIRADI YOTE INAYOTEKELEZWA WILAYANI MKALAMA IWE IMEKAMILIKA' RC SERUKAMBA '
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, amefanya ziara ya kutembelea na kukagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika Wilaya ya Mkalama na kutoa agizo kwa viongozi na wasimamizi miradi hiyo katika Halmashauri ya Wilaya kuhakikisha ifikapo Juni 20, mwaka huu iwe imekamilika.
Pia ametoa agizo baadhi ya miradi kama ya ujenzi wa shule mpya za msingi ujenzi uwe unafanyika kwa saa 24 na kuongeza idadi ya mafundi ili kuongeza kasi ya ujenzi na kumwagiza Meneja wa Shirika la Umeme (TANESCO) Wilaya ya Mkalama kupelekea umeme kwenye miradi hiyo ili mafundi wafanye ujenzi muda wote.
Mhe. Serukamba ametoa agizo hilo leo (Mei 26, 2023) katika siku ya kwanza ya ziara yake wilayani Mkalama ambapo ametembelea na kukagua miradi sita ambayo ni ujenzi wa shule mpya za msingi, ujenzi wa mabweni, vyumba vya madarasa, vyoo, zahanati na Hospitali ya Wilaya ya Mkalama.
Serukamba alianza kwa kutembelea kikundi cha watu wenye ulemavu Iguguno kinachojishughulisha na biashara ndogondogo, ukamlilishaji wa ujenzi wa zahanati ya kijiji cha Lukomo na ujenzi wa shule mpya ya msingi Ishenga.
Akiwa katika mradi wa ujenzi wa shule mpya ya Ishenga alimwagiza mhandisi wa ujenzi na Miundombinu wa Wilaya kuhakikisha kila siku awe anafika kwenye mradi huo kukagua kuona ujenzi unavyoendelea na atembelee kila jengo kujua changamoto ziliyopo kwa mafundi na kuzitatua.
“Mhandisi wa Wilaya kwanza wewe ubaki hapa hapa kwenye mradi hakuna haja ya kuendelea na mimi kwenye ziara baki usimamie tutanataka mradi huu ifikapo Juni 7, mwaka huu ujenzi wa shule hii uwe umekamilika,” alisema Serukamba.
Katika mradi wa ujenzi wa nyumba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashuari ya Wilaya ya Mkalama ambayo serikali imeshatoa Sh. Milioni 300, ameagiza ifikapo Juni 20, mwaka huu ujenzi uwe umekamilika na kukabidhiwa kwa serikali.
Mkuu wa Mkoa akiwa katika mradi wa ujenzi wa matundu ya vyoo 17 shule ya msingi Mazilinga amemwagiza Afisa Elimu Shule za Msingi kuhakikisha anasimamia kwa karibu ujenzi huo na uwe umakalimika ifikapo Juni 19, mwaka huu.
Aidha, Serukamba ametoa agizo la jumla kwa Mhandisi wa Ujenzi Mkoa katika shule tisa mpya za msingi zinazojengwa kwenye halmashauri kutokana na fedha za mradi wa BOOST kuanzia Jumatatu wiki ijayo aanze kuzitembelea na kuangalia maendeleo ya ujenzi na siku Ijumaa ampelekee ripoti.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.