Watendaji wa Serikali katika ngazi ya Kata, Tarafa na vijiji mkoani Singida wametakiwa kutumia muda wao mwingi katika kusimamia ujenzi wa vyumba vya madarasa unao endelea katika maeneo mbalimbali mkoani hapa ili kufanikisha ujenzi huo kwa wakati na kwa viwango vilivyokusudiwa.
Mkoa wa Singida umepokea fedha za UVIKO 19 kiasi cha Sh.Bilioni 13.24 kwa upande wa elimu ili kujenga vyumba vya madarasa 632 ambapo vyumba 330 ni kwa ajili ya shule za sekondari na 330 shule za msingi pamoja na mabweni mawili (2) kwa ajili wenye mahitaji maalum ikiwa ni matarajio ya Serikali kwamba fedha hizo zitasimamiwa na kukamilisha ujenzi huo.
Kauli hiyo imetolewa na Katibu Tawala wa Mkoa wa Singida Dorothy Mwaluko jana tar. 29.11.2021 wakati akikagua miradi mbalimbali ya ujenzi wa vyumba hivyo katika Wilaya ya Mkalama ambapo amebainisha kwamba hali ya ujenzi inaendelea vizuri na vyumba vingi vimefikia katika hatua ya lenta na vingine vikisubiri kupauliwa.
Aidha katibu Tawala Mwaluko amewataka viongozi mbalimbali wa Serikali wakiwemo watendaji wa vijiji, Kata na Tarafa kuhakikisha haipiti siku bila kujua kinachoendelea katika miradi hiyo ambayo inatakiwa kukamilika kabla ya tarehe 15 Desemba mwaka huu.
Akiwa katika miradi hiyo Dorothy Mwaluko ametuma ujumbe kwa wakuu wa shule zote mkoani Singida zenye miradi inayotumia fedha za UVIKO 19 kuhakikisha wanajenga kwa kufuata michoro iliyokubalika na kuhakikisha kwamba wanafanya mawasiliano ya karibu na wahandisi wa Halmashauri za wilaya zao endapo kuna umuhimu wa kufanya hivyo ili kulinda ubora na viwango vilivyotajwa na wataalamu hao.
Katika hatua nyingine amewataka viongozi kuhakikisha wanazishirikisha kamati za ujenzi wa madarasa na kamati za mapokezi ya vifaa vya ujenzi, kiasi cha fedha zilizokuja na namna ya matumizi ya fedha hizo kama sehemu ya kuweka uwazi na kutengeneza dhana ya ushirikishwaji.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Sophia Kizigo amesema wilaya imepokea fedha kwa ajili ya ujezi wa vyumba vya madarasa 63 na ya shule shikizi 16 ambazo kwa jitihada wanazofanya vyote vitakamilika Kwa wakati.
Aidha Mhe. Kizigo amesema hali ya ujenzi kwa sasa inaendelea vizuri baada ya kumaliza changamoto ya upatikanaji wa vifaa vya ujenzi ambavyo vilikuwa havipatikani kwa kuwa zoezi la ujenzi wa vyumba vya madarasa unafanyika nchi nzima hivyo kusababisha changamoto za upatikanaji wa vifaa hivyo.
Amesema kwa sasa Wilaya imeshanunua vifaa vyote vinavyo hitajika katika ujenzi huo ambapo amebainisha kwamba 85% ya majengo yamefikia hatua ya kufungwa lenta wakati asilimia 15% vinafungwa mkanda wa katikati ili kuondoa nyufa zinazoweza kutokea.
" mbao zitakazotumika kwa wilaya nzima tayari zimeshafika kilichobaki ni kuzisambaza kwenye shule mbalimbali na mpaka kufikia kesho jioni mabati nayo yatakuwa yamefika". alibainisha Dc Kizigo.
Pia ametuamia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mama Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha hizi katika Wilaya ya Mkalama jambo ambalo amesema limeondoa kabisachangamoto ya uhaba wa madarasa.
Ziara hiyo imehusisha viongozi mbalimbali wa Wilaya ya Mkalama ambapo walitembelea Miradi katika shule ya Ibaga Kata ya Ibaga ambapo kunajengwa vyumba vitano (5) vya madarasa, Shule ya Sekondari Nduguti kunakojengwa vyumba viwili (2), Shule ya Sekondari Gunda Kata ya Ilunda kunakojengwa chumba kimoja, Shule ya Sekondari Grace Mesaki kunakojengwa chumba kimoja, Kikhonda Sekondari kwenye ujenzi wa vyumba vitatu (3) na Shule ya Sekondari Iguguno kunakojengwa vyumba vine (4) vya madarasa.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.