Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula ameipongeza jamii ya wawindaji ya wahadzabe iliyopo wilaya ya Mkalama mkoani Singida kwa utayari iliyouonesha wa kutambua na kukubali kupimiwa maeneo yao na kupatiwa hatimiliki za kimila.
Jumla ya hatimiliki za kimila mia moja (100) zikiwemo 26 zinazomilikiwa kwa pamoja kati ya mke na mume zimetolewa kwa jamii ya wawindaji ya Wahadzabe ikiwa ni hatua kubwa kutokana na jamii hiyo kujishughulisha zaidi na uwindaji, utafutaji matunda, urinaji asali na uchimbaji mizizi.
Dkt Mabula alisema, hatua hiyo inaonesha nia na dhamira njema waliyonayo ya kutaka kuyalinda maeneo yao wenyewe na kwa kushirikiana na serikali.
‘’Hakika hizi ni salamu na ujumbe wa Rais Samia Suluhu Hassan Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa jamii ya wawindaji inaungana naye na mkoa tayari kwenda naye sambamba katika kuletea watu wote maendeleo’’ alisema Dkt Mabula.
Akizungumza na wananchi wa jamii ya wawindaji ya Wahadzabe katika kijiji cha Munguli kata ya Mwengeza wilaya ya Mkalama Juni 11, 2022 alisema, jamii hiyo ni miongoni mwa jamii ndogo nchini ambayo iko katika hali ya kupoteza ardhi wanayoimiliki kutokana na jamii nyingine kuingia na kufanya shughuli zisizoendana na tamaduni za jamii hiyo jambo alilolieleza linahatarisha ustawi na maisha na desturi za Wahadzabe.
‘’Katika miaka ya hivi karibuni jamii hii imekuwa ikikabiliwa na tishio la kutoweka na kupoteza uhalisia wa maisha yao baada ya jamii nyingine kuingia katika maeneo ya mapori ya asili yanayotumiwa na Wahadzabe kwa ajili ya kufanya shughuli za ufugaji, ukulima na hata upasuaji wa mbao jambo alilolieleza limekuwa tishio kwa kiasi kikubwa kwenye jamii hii’’ alisema Dkt Mabula
Alitolea mfano wamatishio kwa jamii hiyo kuwa ni pamoja na kupotea kwa makazi ya asili yanayojengwa kwa nyasi kavu chini ya matawi ya miti, wanyama kutoweka, mizizi na matunda kupotea kutokana na mabadiliko ya tabia nchi na shughuli nyingine ambazo hazilindi uoto wa asiili wa mapori hayo.
Hata hivyo, alisema kuwa, kwa kutambua athari iliyopo mbele ya jamii hiyo ya wahadzabe, Serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali imekuwa ikitafuta njia bora ya kulinda jamii hiyo pamoja na jamii nyingine zinazofanana ili kuhakikisha inajenga jamii yenye usawa kwa watumiaji wote wa rasilimali za ardhi nchini.
Aidha, katika kuleta usawa Serikali imeendelea na program mbalimbali kuhakikisha kila kipande cha ardhi kinapimwa kwa lengo la kuruhusu usawa na ustawi siyo tu wa binadamu bali wa viumbe vyote vyote hai nchini.
‘’Ukiachilia mbali ukuzaji na uhifadhi wa tamaduni za jamii ya uwindaji kiloichonifurahisha zadi ni kuona jinsi jamii ilivyostaarabika kwa kuona na kuelewa umuhimu wa baba na mama kumiliki ardhi kwa pamoja , kwa hili niwapongeze’’ alisema Dkt Mabula.
Mkuu wa wilaya ya Mkalama Sophia Kizigo alisema, jamii ya Wahadzabe katika eneo hilo la kijiji cha Munguli kata ya Mwengeza imekuwa ikikabiliwa na changamoto ya mgogoro wa mpaka unaosababisha maeneo wanayotegemea kwa shughuli zao kuharbiwa.
‘’Changamoto kubwa ya hapa, jamii ya Wahadzabe vyakula wanatoa porini, wanakula asali na nyama zakuwinda na misitu ikiharibiwa au maeneo wanayotegemea kupata vyakula yanapoharibiwa ni changamoto kubwa, hata hivyo niwapongeze kwa uvumilivu wao’’ alisema Kizigo.
Akiongea kwa niaba ya jamii hiyo Chifu wa jamii ya wahadzabe ameishukuru Serikali ya awamu ya sita kwakuwajali na kupima maeneo yao hivyo kuongeza kuwa watatumia maeneo ya katika shughuli za Maendeleo na kuacha tabia ya kuhamahama .
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.