Jamii ya Wahadzabe inayoishi Kijiji cha Munguli Kata ya Mwangeza wametakiwa kutumia hati miliki walizopewa kujiletea maendeleo na kushirikiana katika kutunza msitu wa Asili wa wahadzabe ili kunufaika na msitu huo unaowapatia Matunda pori, mizizi ,nyama na asali ambayo ilikuwa shauku yao ya muda mrefu.
Hayo yamesemwa na Diwani kata ya Mwangeza Mhe.Bosco Samweli ambaye pia ni Makamu mwenyekiti wa halmashauri ya wilaya ya Mkalama wakati akikabidhi hati hizo kwa jamii ya Wahadzabe iliyofanyika katika Kijiji cha Munguli, Kitongoji cha kipamba wilaya ya mkalama.
Aidha Mhe.Bosco amesema kuwa hati hizo zikawe chachu ya wao kulinda Msitu wa asili ambao ulifanyiwa mchakato wa matumizi bora ya ardhi na hatimaye umekamilika hivyo kuwataka kuendeleza ushirikiano wao katika kuulinda na kuheshimu maeneo tengefu ikiwa ni pamoja na maeneo ya makazi, malisho, vyanzo vya maji pamoja na eneo la msitu.
Afisa Ardhi wilaya ya Mkalama Bw.Imikugwe Mwanitu amesema kuwa kupata hati hizo ni kuendelea kutoa hati za kimila kwa jamii hiyo na kwa mtu mmoja mmoja ambaye anataka ardhi yake ifanyiwe mpango wa matumizi bora ya Ardhi hivyo kuwataka viongozi wa Kijiji cha Munguli kutunza cheti hicho katika hali ya usalama kwa manufaa ya kizazi kijacho.
Katika hatua nyingine Afisa Mazingira wilaya ya Mkalama Bw.Amon Sanga amesema Halmashauri ya wilaya ya Mkalama kwa kushirikiana na timu ya shirika la ujamaa wa jamii katika kulinda raslimali (Ujamaa Community Resource Team) walianza mchakato wa kupata hati tangu mwaka 2018/2019 ambapo walianza upimaji wa maeneo yaliyotengwa hadi kukamilisha mchakato wa utoaji wa hati wa Kijiji na Msitu wa Munguli ilikurahisisha upatikanaji wa hati miliki kwa maeneo mengine katika kutimiza takwa la kisheria.
Naye Afisa Uwanda kutoka shirika la ujamaa wa jamii katika kulinda raslimali (UCRT) Bw Julius Mando ameitaka jamii hiyo kutunza msitu wa Asili kwa faida ya jamii na kuhakikisha Ardhi yao inabaki salama na kupata manufaa kama wanavyopata jamii ya wahadzabe inayoishi Mkoa wa Manyara kupitia msitu wao walioingia mkataba na shirika la Carbon Tanzania.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.