Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Moses Machali amewataka wasimamizi na wakusanya mapato wote kuhakikisha wanakuwa waaminifu katika kazi yao na kudhibiti mianya yote ya upotevu na utoroshaji wa mapato unaosababisha hasara kwa Halmashauri.
Ameyasema hayo mapema leo wakati akiongea na wakusanya mapato na Timu ya Mapato ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama (TASK FORCE) katika ukumbi wa Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Mkalama.
‘’Leo tarehe 28 mwezi wa pili nakutana nanyi timu inayohusika na ukusanyaji wa mapato wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama tumegundua kwamba ipo mianya ya upotevu wa mapato na zipo taarifa, usisubiri mpaka tuje tukufuate ukakamatwa utakuwa umepoteza kazi, hivyo utamuaga Mkeo utamuaga mumeo na Watoto wako, itakuwa ni hasara na vilio katika familia yako’’ Alisisitiza Mhe. Machali
Aidha, amewataka watumishi hao kuwa waaminifu na kazi waliyopewa na kuaminiwa na Serikali kuhakikisha kila pesa inayopatikana inawekwa Benki ili kuepusha ushawishi utakao pelekea kutumia fedha hizo .
‘’Hakikisheni mnakuwa waaminifu katika kazi na kila pesa mnayokusanya inaingia kwenye kapu letu la Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama inayoongozwa hapa na Bi. Asia Messos na ole wake atakayeingia kwenye kumi na nane tutamshambulia kama Mpira wa kona’’ Aliongeza Mhe. Machali
Sanjari na hayo amemtaka Afisa mapato kuwa mbunifu katika kuibua vyanzo vipya vya mapato ili kuharakisha pato la Wilaya na kuagiza kuchukuliwa hatua kali za kisheria kwa kampuni zote za ujenzi wanazofanya shughuli wilayani hapa ambazo hazilipi Ushuru wa Madini ya Ujenzi.
Bi. Elizabeth Rwegasira, Katibu Tawala wa Wilaya ya Mkalama pamoja na Mkurugenzi Mtendaji Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Bi. Asia Messos nao wamesisitiza uaminifu na umakini katika utendaji kazi kwa maslahi mapana ya Wilaya ambapo wamesema kuwa uadilifu na ni zamu ya kazi utawapelekea kuendelea kuaminiwa na kupewa nafasi kubwa zaidi.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.