Mkuu wa Wilaya ya Mkalama, Mhe. Moses Machali amewataka Watumishi wa Idara zote na Vitengo na Taasisi zilizopo Mkalama kila mmoja kwa nafasi yake kufanya kazi kwa weledi, kuacha mzaha, kuheshimu kazi huku wakizingatia Sheria na Taratibu zilizowekwa katika kufuata maelekezo halali wanayopewa yasiyo athiri taratibu za kazi.
Ameyasema hayo mapema leo February 9, 2023 katika kikao kazi kilichojumuisha, Wakuu wa Idara, Vitengo, Taasisi na Watendaji wa Kata katika Ukumbi wa Ofisi za Mkuu wa Wilaya ya Mkalama kikiwa na lengo la kukumbusha majukumu na wajibu wa kila mmoja kufanya kazi kwa bidii kwa kuzingatia Taratibu na Sheria za kazi.
‘’Tumekuja hapa kukumbushana ni nini tunachotakiwa kufanya, kupeana muelekeo bila kutoka nje ya Misingi iliyojengwa kwenye Katiba yetu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania’’ Alisisitiza Mhe. Machali.
Mhe. Machali, ameongeza kuwa kila mmoja kwa nafasi yake ya taaluma anatakiwa kufanya majukumu kwa weledi na kwa kushirikiana pia kuwa tayari kupokea mabadiliko ya kifkra ya namna dunia inavyoenda kutokana na kukua kwa Sayansi na Tekinolojia .
Pamoja na hayo, aliwataka kutumia nafasi zao kutatua changamoto za Wananchi kwa kwenda Vijijini kubaini Migogoro ya Ardhi na namna walivyoishughulikia pia kutoa elimu kwa jamii kushiriki katika shughuli za Maendeleo ili kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Serikali.
‘’wakuu wa Idara tokeni ofisini nendeni kwa Wananchi mkashughulikie matatizo ya Wananchi, ipende na kuiheshimu nafasi yako uliyonayo na kuitendea haki ‘’ Aliongeza Mhe. Machali.
Sanjari na hayo Mhe. Machali alimwelekeza Mkurugenzi Mtendaji kushirikiana na Timu yake kuhakikisha wanaongeza ukusanyaji wa mapato na kudhibiti mianya yote ya utoroshaji na ukwepaji wa kulipa kodi Pamoja na kuwataka wakandarasi wanaopata tenda Wilayani hapa kuhakikisha wanalipa ushuru wa Madini ya Ujenzi.
"Mkurugenzi hakikisha unaweka utaratibu mzuri na timu yako kufuatilia ushuru wa kila chanzo, nimeambiwa hapa mna vyanzo kumi na saba(17) vya mapato kama ni mnadani hakikisheni mnakusanya kikamilifu, kama ni Magetini hakikisheni mnasimamia vizuri’’ Alisema Mhe. Machali
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Bi. Asia Messos ameahidi kushughulikia maelekezo yote waliyopewa leo na Mkuu wa Wilaya ili kuendana na dira na kasi yake na kuhakikisha anawaelekeza Menejimenti yake kushughulikia kero za Wananchi kwa ustawi mpana wa wanamkalama.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.