Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Moses Machali amewataka Wenyeviti wa Vijiji wilayani hapa kufanya kazi kwa weledi pamoja na kuhakikisha wanahamasisha wazazi wenye watoto wenye sifa wanawapeleka shule.
Kauli hiyo ameitoa Januari 21, 2025 wakati wa kikao cha Kamati ya Ushauri ya Wilaya ya Mkalama (DCC) kilichofanyika katika ukumbi wa Sheketela uliopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama.
“Nawasihi nendeni mkahamasishe wazazi wenye watoto wawapeleke watoto wao shule, serikali imeweka mazingira mazuri ya watoto kusoma, hivyo sitegemei kukuta motto mwenye sifa ya kusoma yupo nyumbani” Mhe. Machali
Aidha Mhe. Machali ametangaza kuwachukulia hatua kali wazazi ambao watashindwa kuwapeleka watoto shule “Nitumie nafasi hii kuwajuza kuwa nitaanzisha oparesheni kuwasaka wazazi ambao nitakuta watoto wao wapo nyumbani ili hali wanasifa za kujiunga na shule” Mhe. Machali.
Akizungumzia suala la uadilifu kazini, Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe. Machali amewataka Wenyeviti wa Vijiji wilayani hapa kujiepusha na masuala ya rushwa, kuuza ardhi za vijiji kiholela pamoja na kufanya kazi kwa ajili ya wananchi.
“Wananchi wamewachagua kwa ajili ya kuwatumikia, sitategemea muwe chanzo cha migogoro ya ardhi huko katika vijiji vyenu lakini sitegemei kusikia mnakuwa chanzo cha mmonyoko wa maadili, nendeni mkafanye kazi kwa ajili ya wananchi na taifa kwa ujumla.” Mh. Machali
Vile vile Mkuu Mhe. Machali amewakumbusha Wenyeviti wa Vijiji kuhakikisha wanafanya vikao mara kwa mara ili kusikiliza na kutatua kero mbalimbali zinazowabili wananchi katika vijiji vyao.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.