Baraza la Madiwani limefanya, maamuzi ya kumfukuza kazi Mtumishi mmoja, limetoa Onyo kwa kwa Mtumishi mmoja na kumshusha Cheo Mtumishi mmoja baada ya kupitia mashauri ya kinidhamu kwa watumishi hao watatu.
Maamuzi hayo yamefanyika katika Mkutano wa Halmashauri wa robo ya pili kwa mwaka wa fedha 2022-2023 uliofanyika leo Machi 16, 2023, ambao ulipitia na kujadili taarifa za robo ya pili ambazo ziliwasilishwa na Wenyeviti wa Kamati za Kudumu za Halmashauri.
Pamoja na kupitia na kujadili taarifa za utekelezaji wa shughuli za Serikali za robo ya pili Mkutano wa Halmashauri ulihitimisha mashauri ya kinidhamu na kufanya maamuzi ya kumfukuza Mtumishi mmoja, limetoa Onyo kwa Mtumishi mmoja na kumshusha cheo Mtumishi mmoja.
Akiwasilisha maamuzi ya Kamati ya Baraza zima ambalo lilijigeuza kama Kamati Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Mhe. James Mkwega ameeleza kuwa
“waheshimiwa wajumbe tuliwaomba mtupishe kwa muda ili Baraza lijigeuza kuwa Kamati ya Utumishi na hapa tulikutana na mashitaka matatu ya Watumishi, Mtumishi wa kwanza ni Mtendaji wa Kijiji cha Kidarafa lakini siyo huyu aliyepo sasa nisahihishe kabisa. Baraza baada ya kukaa na kuchunguza na kujiridhisha tuhuma zake na utetezi alioutoa kwenye Kamati ya Fedha imetoa maamuzi yafuatayo; Baraza limemuamuru kurudisha kiasi cha Shilingi 601,000/= alizozitumia huyu Mtendaji kinyume na utaratibu ndani ya miezi mitatu na kupewa Onyo. Mtumishi wa pili tumesikiliza tuhuma za Afisa Elimu vielelezo baada ya kujiridhisha kama Baraza, Baraza limeamua kumshusha cheo na kuamua abadilishiwe kituo cha kazi wakati akiwa kwenye muda wa matazamio. Shitaka la tatu, Baraza limejiridhisha kwa kina juu ya Afisa Mtendaji wa Kijiji cha Maziliga na kufanya maamuzi yafuatayo; Baraza limeamua kutoa adhabu ya juu kabisa kwa Mtendaji huyu baada ya kujiridhisha na kuona tuhuma zake alizotuhumiwa ni nzito lakini bado hakuonyesha mabadiliko ya tuhuma hizi baada ya kukutana na Kamati ya Fedha kwa hiyo Baraza limemfukuza kazi Mtendaji huyu kwa kushindwa kusimamia majukumu yake” Aliongeza Mhe. Mkwega
Pamoja na hayo Mhe. Mkwega amewataka watumishi kuwa waadilifu na kufanya kazi kwa kuzingatia Sheria na Taratibu za kazi ili kuepuka hatua za kinidhamu zinazoweza kuchukuliwa dhidi yao .
Aidha, aliongeza kwa kuwataka watumishi kuwa na ratiba nzuri za kazi zao na kuacha kusubiri Maazimio ndipo waanze kutekeleza wajibu wao.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.