Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama, Mhe. James Mkwega amempongeza Mkurugenzi Mtendaji na Menejimenti ya Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama kwa kuandaa bajeti nzuri iliyozingatia vipaumbele mbalimbali iliyojikita kwenye miradi ya
maendeleo ya wananchi inayoakisi uhalisia.
Ametoa pongezi hizo mapema leo January 27, 2023 wakati akifungua kikao maalumu cha Baraza la Madiwani la kupitia na kujadili mapendekezo ya bajeti ya Halmashauri kwa Mwaka wa fedha 2023/2024.
‘’ kwa kweli ninakupongeza Mkurugenzi Mtendaji na timu yako mmeandaa bajeti nzuri inayozingatia vipaumbele na mahitaji ya Halmashauri na kwa namna bajeti hii ilivyo ina kwenda kuleta mahitaji ya maendeleo ya Wanamkalama’’aliongeza Mhe. Mkwega.
Pamoja na Bajeti hiyo nzuri Mhe. Mkwega alisema kuna maeneo amabayo hayajapangiwa bajeti kama vile kukarabati maboma yaliyochakaa na barabara hivyo aliwaomba wanaohusika kuangalia kwa jicho la Tatu ili maeneo hayo yatengewe bajeti.
Mhe. Mkwega aliwatia moyo watumishi kila mmoja kwa nafasi yake kufanya kazi kwa bidii huku wakiendelea kudumisha upendo na ushirikiano ili kuchochea maendeleo ya Halmashauri, huku akiwataka kusimamia vyema miradi inayotolewa na Serikali na hatimaye kukamilika kwa wakati.
Sanjari na hayo Mhe. Mkwega alimtaka Mkurugenzi kupitia Ofisi ya Mipango kuandaa taarifa ya utekelezaji kwa kila kata zenye miradi na kuzisambaza kwa Madiwani , kubainisha thamani ya mradi na utekelezaji wake ni kwa muda gani.
Awali akisoma Rasimu ya Mpango wa bajeti Kaimu Afisa Mipango Bw. Daniel Tesha alisema kuwa kwa mwaka wa fedha 2023/2024 Halmashauri ya Wilaya ya Mkalama imejipanga kukusanya na kutumia jumla ya Shilingi 27 ,073,624,492.00 kwa ajili ya Mishahara na Matumizi Mengineyo.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mkalama, Mhe. Lameck Itungi alisema kuwa kazi ya Chama cha Mapinduzi ni kuhakikisha inasimamia Ilani ya Chama Cha Mapinduzi katika kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo wilayani na kuwataka Madiwani kwenye Mikutano yao kusema mazuri yaliyofanywa na Serikali ya awamu ya Sita.
‘’Ifike wakati sasa Waheshimiwa Madiwani muhubiri maendeleo yaliyofanywa na serikali ya awamu ya sita kwenye Kata zenu kuwaambia wananchi mazuri yanayofanywa na Serikali ya Chama cha Mapinduzi’’ Aliongeza Bw. Itungi
Akiongea kwa niaba ya Mkurugenzi , Afisa Elimu Sekondari Mwl . Said Kalima amesema atahakikisha bajeti hii inasimamiwa kwa weledi mkubwa kama ilivyokuwa kwa bajeti iliyopita na kuhakikisha wanaongeza makusanyo ya Halmashauri na kuvuka lengo na kuongeza kuwa watashirikiana na Wataalamu wake kusimamia fedha kwa ajili ya miradi ya maendeleo zinafanya kazi iliyokusudiwa na kukamilika kwa wakati.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.