Juni 14 ya kila Mwaka huwa yanafanyika maadhimisho ya siku ya Watu wenye ulemavu wa Ngozi maarufu kama Albino ambapo kwa Mkoa wa Singida yamefanyika katika Wilaya ya Iramba.
Mgeni rasmi wa maadhimisho hayo alikuwa ni Mkuu wa Mkoa wa Singida Mhe: Rehema Nchimbi ambaye aliwakilishwa na Mkuu wa Wilaya ya Mkalama Mhe: Mhandisi Jackson Masaka ambapo alianza hotuba yake kwa kuwashukuru wananchi wa Wilaya zote za Mkoa wa Singida waliojitokeza katika maadhimisho hayo.
“Najua wengi wenu mmeacha shughuli zenu na kuamua kuja kushiriki na wenzetu maalbino, Nawashukuru sana na naomba muendelee kuwaonesha ushirikiano huu” Alisema Mhe: Nchimbi.
Aliongeza kwa kuzishukuru mamlaka za ulinzi na Usalama kwani kwa kipindi kirefu Mauaji ya Watu wenye Ualbino hayajasikika tena na kuziomba ziendelee kuimarisha Uinzi dhidi ya watu hao ambao alisisitiza kuwa hawana tofauti na Mtu mwingine yoyote.
Akijibu sehemu ya Risala ya Chama cha watu wenye Ualbino Tanzania kuhusu kuwezeshwa kiuchumi, Mhe: Nchimbi amesema kuwa ni vyema chama hicho kiangalie na kuwekeza kwenye fursa mbalimbali za uzalishaji mali kama vile Kilimo, Ufugaji, ushonaji na nyinginezo ili kujihakikishia faida kubwa pindi kitakapouza mavuno yatokanayo na sekta hizo.
“Serikali itahakikisha inaunda kamati za kuratibu watu wenye ulemavu katika ngazi zote kuanzia ngazi ya kitongoji mpaka Wilaya” Aliongeza Mhe: Nchimbi.
Aidha Mhe: Nchimbi aliagiza takwimu za watu wenye ualbino zihuishwe mara kwa mara ili kuuwezesha Mkoa kutekeleza shughuli mbalimbali zinazohusu ustawi wao.
Mkoa wa Singida una jumla ya watu wenye ulemavu wa ngozi ( Maalbino) 419 ambapo Wilaya ya Manyoni wapo 73, Iramba 87, Singida (vijijini) 85, Singida Manispaa 57, Mkalama 29, Ikungi 22 na Itigi 36.
Kauli Mbiu ya Mwaka huu ya maadhimisho ya Siku ya Kuwajali watu wenye Ulemavu wa Ngozi (maalbino) ni “UMUHIMU WA TAKWIMUNA TAFITI KWA USTAWI WA WATU WENYE UALBINO”.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.