Katika kupambana na kichaa cha Mbwa ndani ya wilaya ya Mkalama ,Idara ya Mifugo kwa kushirikiana na Taasisi isiyo ya kiserikali ya Education for African Animals Walfare (EAAW) inayojishughulisha na haki na ustawi wa Wanyama Nchi wamefanya chanjo kwa Vijiji vya Ilunda na Matongo ambapo kwa vijiji hivyo wamechanja Mbwa wapatao 303.
Zoezi hili limefanyika mwishoni mwa mwezi wa 11 .2021 katika Kijiji cha Ilunda Kata ya Ilunda na Kijiji cha Matongo Kata ya Matongo wilaya ya Mkalama Mkoani Singida.
Akiongea katika zoezi hilo Afisa Mifugo wilaya ya Mkalama Bw.Dotto Michael amesema zoezi hilo ni kutekeleza takwa la kisheria chini ya sheria Na. 17 ya mwaka 2003 ya udhibiti wa magonjwa ya wanyama na sheria Na.19 ya 2008 ya haki na ustawi wa Wanyama Rafiki .
Aidha ameongeza kuwa zoezi hilo muhimu hufanyika kwa lengo la kupunguza ugonjwa wa kichaa cha Mbwa ili kupunguza hasara kwa wafugaji pindi wanyama wao wanapopata kichaa kuwapoteza na kugharamikia fedha nyingi pindi Mbwa wanapowang’ata watu kutokana na matibabu yake kuwa ghali.
Katika hatua nyingine Bw.Dotto amewataka wafugaji kujitokeza kwa wingi kupeleka Mbwa wao kupatiwa chanjo pindi wanapopata taarifa ili kutokomeza kabisa kichaa cha Mbwa wilayani Mkalama ambapo kwa mwaka 2021/2022 wanatarajia kufikia 2% ya kupunguza Mlipuko wa kichaa cha Mbwa ukilinganisha na mwaka 2019 ambapo Mlipuko wa kichaa cha Mbwa ulikuwa ni 8%.
Mkurugenzi wa Taasisi ya EAAW inayojihusisha na ustawi wa Wanyama Bw.Ayubu Nnko amesema kuwa Shirika hilo limekuwa likishirikiana na wilaya ya Mkalama tangu mwaka 2019 ambapo kulikuwa na kesi nyingi za Mlipuko wa kichaa cha Mbwa ambapo toka zoezi hilo kuanza kesi hizo zimepungua kutoka 8% mwaka 2019 hadi 4% 2020/2021.
Bw. Nnko amesema kuwa Nchi za Afrika na Tanzania ikiwepo zimekuwa zikitumia Dolla million ishirini kila mwaka kutibu watu wanaopata kichaa cha Mbwa ambapo ametumia fursa hiyo kuwataka wafugaji kuzingatia chanjo hiyo ili kuepuka gharama hizo.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.