MKUU wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba,ameiagiza Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoani kwa kushirikiana na vyama vya wafanyakazi kuhakikisha rushwa ya ngono na unyanyasaji wa kijinsia inatokomezwa katika mkoa huu.
Akizungumza leo (Mei Mosi) 2023 wakati wa sherehe za maadhimisho ya Siku ya wafanyakazi kimkoa zilizofanyika Manispaa ya Singida, amesema tatizo la rushwa ya ngono ni lazima likomeshwe kwenye Mkoa wa Singida.
Serukamba ameliagiza Shirika la Bima mkoa wa Singida kufanya uhakiki wa wafanyakazi ambao Bima zao zimeiva waweze kulipwa na Wakurugenzi wa Halmashauri ambao hawajawalipa watendaji posho za kila mwezi kuanza kulipa posho watendaji wa kata ndani ya miezi mitatu na kutoa taarifa kwake.
"Nichukue nafasi hii kumpongeza Rais Dk.Samia Suluhu Hassan kwa kuona umuhimu wa kuwapandisha madaraja watumishi waliokuwa wanastahili hali ambayo imeleta motisha na tija katika utendaji kazi kwa watumishi ," alisema Serukamba.
Naye Mratibu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA) Mkoa wa Singida,Maria Bange, akisoma risala ya wafanyakazi amesema rushwa ya ngono katika harakati za kutafuta ajira imepungua katika kipindi cha 2022/2023.
Amesema katika kipindi hicho kumekuwa na changamoto kadhaa ikiwamo baadhi ya viongozi kuwaweka ndani wafanyakazi bila Kufuatia utaratibu na sheria za Kazi.
Ameongeza kuwa changamoto nyingine ni nyongeza ya mishahara iliyofanyika mwaka jana haijakidhi matarajio ya wafanyakazi, kutolipwa kwa wakati fedha za Uhamiaji,likizo na malimbikizo ya mishahara kucheleweshwa hadi wengine kustaafu na ucheleweshaji wa pesheni kwa wastaafu.
Ameendelea kutaja Changamoto nyingine kuwa Shirika la Bima kutowalipa watumishi waliokata Bima ya maisha wakati Bima zao zinapoiva,waajiri binafsi kutowasilisha Makato ya asilimia 10 kwenye mifuko ya hifadhi ya jamii,waajiri kutopeleka michango ya hifadhi ya jamii kwa wakati na kusababisha tozo kubwa.
Bange amesema pamoja na changamoto hizo wafanyakazi wanaomba serikali iongeze nyongeza ya kima Cha chini Cha mshahara inayoendana na hali ya uchumi wa sasa,kuhamisha wafanyakazi kuendane na ulipaji wa stahiki zao.
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.