Wakazi wa Kijiji cha Munguli kilichopo Kata ya Mwangeza Wilayani Mkalama wameridhia kutangazwa kwa hifadhi ya Msitu wa Munguli wenye ukubwa wa Hekta 1656, katika Gazeti la Serikali ili kuhakikisha Msitu huo unalindwa na kutunzwa ili uweze kuwapatia manufaa.
Wamefanya maridhiano hayo January 5, 2023 katika mkutano Mkuu wa Kijiji uliofanyika katika Kijiji cha Munguli Kata ya Mwangeza.
Afisa Maliasili Mkoa wa Singida Bw. Charles Kidua aliwaeleza wananchi umuhimu wa kutangazwa kwa Msitu huo katika Gazeti la Serikali kuwa utawapa manufaa makubwa kwani ngazi za juu zitautambua Msitu pamoja na kuwekwa kwa Sheria ndogo za Usimamizi Shirikishi wa Msitu na kupelekea watakao haribu kwa makusudi bila kufuata taratibu kuchukuliwa hatua.
Aidha, Bw. Kidua alitaja faida za utunzaji wa Msitu kuwa ni kupata fedha kwa kunyonya hewa ya ukaa hivyo kupunguza kero ya kutoa michango ya maendeleo mara kwa mara pindi inapojitokeza.
‘’ katika kupambana na mabadiliko ya tabia Nchi kama ilivyokuwa zamani lazima kila mtu ajue umuhimu wa hifadhi ya mazingira na utunzaji wa msitu ambao hivi karibu utatangazwa katika gazeti la Serikali ili Wananchi wa Munguli waweze kunufaika na Msitu huu kama ilivyo kwa jamii ya Wahadzabe waliopo Yaeda chini Mkoani Manyara’’ aliongeza Bw. Kidua.
Mwanasheria wa Wilaya ya Mkalama Bw, Daud Makendi aliwataka wananchi kufuata Sheria na taratibu ili kuepuka kuingia katika makosa ya kisheria ikiwa ni pamoja na kutoa katazo la kuingia na kufanya shughuli zozote za kibinadamu ndani ya msitu bila kupata kibali cha maandishi kutoka kwa Mamlaka husika.
Aidha, Bw. Makendi aliongeza kuwa mtu yeyote atakayekiuka au kwenda kinyume na kifungu chochote cha sheria ndogo atakuwa ametenda kosa na akipatikana na hatia atatozwa faini isiyopungua shilingi elfu Hamsini na isiyozidi Laki moja ikiwa ni pamoja na kulipa fidia ya uharibifu baada ya tathimini kufanyika au kifungo kisichopungua miezi sita na kisichozidi miezi kumi na mbili au vyote faini na kifungo kwa pamoja.
Baadhi ya wananchi waliokuwa kwenye Mkutano huo waliahidi kuulinda na kutunza hifadhi ya Msitu bila kuvunja Sheria ndogo na kuridhia kwa pamoja kuwa msitu wao utangazwe kwenye gazeti la serikali .
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.