Jamii imetakiwa kupinga vitendo vya ukatili kwa watoto na kuripoti vitendo hivyo kwenye vyombo vya sheria na kutoa ushahidi kwa vyombo hivyo ili kusaidia kuchukuliwa hatua stahiki kwa wanaoendelea kufanya vitendo hivyo.
Kauli hiyo imetolewa juni 16 na Remigius Ngole Afisa Tarafa, Tarafa ya Nduguti alipomwakilisha Mkuu wa Wilaya ya Mkalama katika kilele cha siku ya mtoto wa Afrika kilichofanyika katika kijiji cha Iambi Kata ya Ilunda Wilayani hapa.
‘’Bado vitendo vya ukatili kwa watoto vinatishia ustawi kwa watoto wetu, vitendo vya kupigwa , kubakwa , kulawitiwa pamoja na mimba kwa wanafunzi havikubaliki katika jamii, hivyo naagiza vyombo vya dola kuchukua hatua stahiki kwa wote wanaofanya vitendo hivi kwa watoto, hivyo ninatoa rai kwa wananchi kufichua vitendo hivi’’. Aliongeza Ngole.
Ngole aliongeza kuwa migogoro ya ndoa imekua ni chanzo cha watoto kufanyiwa ukatili na kuzalisha tatizo la ongezeko la watoto wa mitaani kwani wanakosa haki za msingi kwakukosa malezi mazuri ya wazazi pamoja na kukosa haki ya kupata elimu hivyo kuwataka wazazi kuepuka migogoro hiyo kwa ustawi wa watoto kwani ni taifa la kesho.
Aidha aliongeza kuwa serikali ya awamu ya Sita imekua ikifanya jitihada za kuhakikisha watoto wanakua kwenye mazingira mazuri na kupata elimu bora na kwakujali hilo imetenga fedha shilling 96,200,000 kwaajili ya ujenzi wa bweni la wasichana shule ya sekondari Malaja ili kupunguza vishawishi kwa watoto wa kike na kutimiza malengo yao .
Awali akimkaribisha Mgeni rasmi Afisa Maendeleo Wilaya ya Mkalama Mohamed Atiki alisema siku ya mtoto wa Afrika huazimishwa kila ifikapo june 16 kila mwaka na Nchi 51 wanachama wa Umoja wa Nchi huru za Afrika(O.A.U).
Atiki aliongeza kuwa lengo la maadhimisho haya ni kukumbuka mauaji ya kinyama waliofanyiwa watoto wa Kitongoji cha Soweto Nchini Afrika Kusini mwaka 1976 hukuTanzania nayo ikiwa kama mwanachama wa Umoja wa Nchi huru za Afrika ilianza kuadhimisha siku ya mtoto wa Afrika mwaka 1991.
Wakisoma risala kwa mgeni Rasmi watoto wa kijiji cha Iambi walianza kwakuishukuru serikali ya awamu ya Sita kuendelea kutoa elimu bila malipo kuanzia Chekechea hadi kidato cha Nne na kuongeza kuwa kwa kipindi cha mwaka Mmoja wameshuhudia juhudi za serikali katika ujenzi wa madarasa kwa kutumia fedha za UVIKO 19 jumla ya madarsa 63 yamejengwa ikiwa kwa shule za Msingi ni madarasa 16 na Shule za Sekondari 47 yaliyogharimu shilingi 940,000,000.
Aidha walisema kuwa pamoja na pongezi hizo wamekua wakikabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwepo kwa matukio ya kufanyiwa ukatili huku wakiomba jeshi la polisi kukamilisha kesi 10 zilizopo kwenye upelelezi pamoja nakuiomba serikali kuhamasisha wazazi kuchangia chakula shuleni kwani inapelekea mahudhurio yao kuwa mabovu pamoja na ufaulu kuwa duni.
Maadhimisho haya huambatana na kauli mbiu mbalimbali ambapo kwa mwaka huu inasema “TUIMARISHE ULINZI WA WATOTO ,TOKOMEZA UKATILI DHIDI YAKE JIANDAE KUHESABIWA’’
OFISI YA MKURUGENZI MTENDAJI HALMASHAURI YA WILAYA YA MKALAMA, 18 MASAKA RD, 43582
Anuani ya Posta: P.o. Box 1007
Simu ya Mezani: 026-2964005
Simu ya Mkononi:
Barua pepe: ded@mkalamadc.go.tz
Copyright ©2018 Mkalama DC . All rights reserved.